ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, February 20, 2018

MACHIMBO YA NYAKAVANGALA KUFUNGULIWA MACHI, 2018

 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na Wachimbaji Madini wa Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mgodini hapo.
 Sehemu ya eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa ambalo lilitembelewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) baada ya kufungwa kufuatia ajali iliyotokea Januari 30, 2018 na kusababisha vifo vya wachimbaji wawili.
 Baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (aliyeshika kipaza sauti) wakati wa ziara yake mgodini hapo.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza mara baada ya kukagua moja ya shimo la dhahabu kwenye Machimbo ya Nyakavangala Wilayani Iringa.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (hayupo pichani) wakati wa ziara yake kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala, Wilayani Iringa. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye shati jeupe) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (wa pili kushoto) walipotembelea eneo linalotumika kuhifadhia marudio ya mchanga wa dhahabu kutoka kwenye Machimbo ya Nyakavangala. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.


Na Mohamed Saif
Serikali imeagiza hadi kufikia Machi 5, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa uwe umekamilika na machimbo hayo yawe yamefunguliwa ili kuruhusu shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa zianze. 

Naibu Waziri wa Madini,  Doto Biteko alitoa agizo hilo Februari 19, 2018 alipofanya ziara kwenye machimbo hayo yaliyoko katika Kata ya Malengamakali, Wilayani Iringa ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao hadi hapo ukaguzi utakapokamilika.

“Serikali haifurahishwi kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Machimbo ya Nyakavangala zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa kutokana na ajali,” alisema.

Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye machimbo hayo ya Nyakavangala Februari 12, 2018 baada ya kutokea vifo vya Wachimbaji Wawili Tarehe 30 Januari, 2018 kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.

Biteko aliagiza wakaguzi kukamilisha zoezi hilo haraka ili shughuli za uchimbaji ziendelee na aliwataka wachimbaji hao kuwa na subira wakati zoezi hilo la tathmini likiendelea ili kuepusha maafa mengine kutokea.

“Mgodi huu hautafunguliwa bila kukamilisha zoezi la ukaguzi kwahiyo ndani ya wiki mbili kutoka leo Wakaguzi wawe wamekamilisha ili mgodi uanze kazi na shughuli za uchumi zilizokuwa zikifanyika mgodini hapa zirejee,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko aliwaonya wachimbaji madini nchini kuacha kufanya shughuli za uchimbaji kwa mazoea badala yake wahakikishe wanafuata sheria na taratibu za uchimbaji salama ili kuepusha ajali inayopelekea kuzorota kwa shughuli za kiuchumi baada ya migodi husika kufungwa.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuifungia migodi inayosababisha ajali na hivyo aliwasisitiza wachimbaji kote nchini kuhakikisha wanafuata ushauri wa kitaalam wanaopewa na Maafisa Madini.

"Maisha ya mtu mmoja ni muhimu kuliko shughuli zote za uzalishaji mgodini, ikitokea kifo kwa sababu ya ajali tunafunga mgodi," alisema Biteko.

Sambamba na hilo, Biteko aliwaagiza Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya machimbo ili kujionea hali ya uchimbaji pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji bora na salama kwa wachimbaji ili kuepusha ajali.

Naibu Waziri Biteko alifanya ziara kwenye machimbo ya Nyakavangala ili kujionea hatua za kiusalama zilizofikiwa tangu kufungwa kwa machimbo hayo kufuatia matukio matatu ya ajali yaliyotokea kwa nyakati tofauti ambayo yalisababisha vifo vya Wachimbaji Wanne.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa, Robert Masunya ilielezwa kuwa, tukio la kwanza la ajali lilitokea Juni 12, 2017 na kusababisha kifo cha Mchimbaji Mmoja, la pili lilitokea Novemba 30, 2017 na kisababisha kifo cha Mchimbaji Mmoja na tukio la tatu lilitokea Januari 30, 2018 na kusababisha vifo vya wachimbaji wawili.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, Kamati za Ukinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya ya Iringa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.