ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 16, 2011

UDOM HAKUKALIKI WANAFUNZI 9,000 WATIMULIWA

ZAIDI ya wanafunzi 9,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamefukuzwa kwa muda usiojulikana kuanzia jana kwa madai ya kuhamasisha mgomo usio halali.Habari zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kuwa wanafunzi hao ni wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Sayansi Asilia. Walitakiwa kuondoka chuoni hapo kabla ya saa 8:00 mchana.Kufukuzwa huko kumekuja siku mbili baada ya kuanzisha maandamano yaliyoshinikiza kujiuzulu kwa viongozi waandamizi wa Serikali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwa madai kwamba wamewadanganya kuhusu malipo yao ya masomo kwa vitendo.

Msimamo wa wanafunzi
Wakizungumza mara baada ya agizo hilo jana baadhi ya wanafunzi hao walisema kuwa hawaoni tabu kufukuzwa wakisema wao ni waathirika wanaotumika kwa maslahi ya wengine.

Walisema kuwa kufukuzwa kwao ni kwa ajili ya kudai maslahi ambayo wamekuwa wakiyatafuta wakati wote bila ya mafanikio na kwamba kama itabidi itakuwa bora waondoke.

“Sisi tunaondoka na wenzetu wengine walishaondoka katika Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta kwa hiyo kwa hali hii lazima chuo chote kitafungwa maana hali inakokwenda chuoni hapa ni siasa tupu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao na kuongeza: “Ni bora turudi nyumbani kwa kuwa huwezi kusoma bila ya kufanya mafunzo kwa vitendo. Ni bora tukae nyumbani tu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao huku akiungwa mkono na wenzake.

Wanafunzi wa Kitivo cha Teknolojia ya Habari na Elimu Angavu walifukuzwa baada ya kugoma wakitaka walipwe fedha kwa ajili ya vifaa vya kujivunzia kwa vitendo.


habari zaidi tembelea www.mwananchi.co.tz

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.